Hashim Mgandilwa, Mkuu wa Wilaya wa Kigamboni
Mgandilwa ameyasema hayo katika kipindi cha SUPAMIX kinachorushwa na East Africa Radio wakati akijibu maswali ya wananchi na kueleza namna alivyojipanga pamoja na watendaji wake kuwahudumia wananchi.
“Watanzania wengi wanapenda kuishi Kigamboni na hili limejidhihirisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huu kila aliyekuwa ananipa pongezi alikuwa ananiambia nisimsahau kiwanja nikapata uelewa ni kiasi gani watu wanapatamani Kigamboni” Amesema Mgandilwa.
Aidha Mgandilwa amesema baada ya kufunguliwa kwa daraja la Kigamboni na vivuko kufanyiwa marekebisho kwa sasa huduma za usafiri zimeimarika kiasi ila jambo ambalo anapambana nalo ni kuhakikisha wilaya yake inakuwa na stendi kubwa ya magari jambo ambalo li[po kwenye mikakati.
Kuhusu suala la ulinzi na usalama Mkuu huyo wa Wilaya ameonesha wasiwasi wake kutokana na wilaya hiyo kuwa na mapori mengi ambayo ni rahisi kwa wahalifu kujificha na kupanga mikakati, hivyo amewasihi wananchi kuwa na moyo wa kizalendo kwa kuwasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukabiliana na makundi ya kihalifu.
Pamoja na hayo Mgandilwa amesema halmashauri ya wilaya yake imejipanga katika kuhakikisha huduma za kijamii zinaimarika kwa wananchi ili watu wengi wazidi kuingia Kigamboni na kufanya shughuli mbalimbali jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.