Jumanne , 18th Oct , 2016

Shirika la Mpango wa Chakula,WFP limechangia karibu dola milioni sitini kwa uchumi wa Uganda kupitia ununuzi wa chakula na ujenzi wa maghala ya chakula nchini humo.

Moja ya mashamba ya ndizi ambayo ni zao la chakula nchini Uganda

WFP imesema, imenunua tani za nafaka zaidi ya 97,000 zenye thamani ya dola milioni 36 mnamo mwaka huu pekee kwa ajili ya kusaidia maelfu ya wakimbizi na wananchi wakiwemo watoto wanaokabiliwa na utapiamlo.

Pia imetoa dola milioni 14 kwa makampuni ya usafirishaji zaidi ya 41, huku dola milioni 7.8 zikitumiwa katika ujenzi wa maghala ya chakula ya Tororo na Kampala pamoja na maghala mengine 12 kote nchini.

Mike Sackett, Kaimu Mkurugenzi wa WFP, Uganda amesema, chakula kilichonunuliwa humo nchini kimekuwa kikitumiwa kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa walio katika uhitaji katika kanda nzima wakiwemo wale nchini Sudan Kusini na Ethiopia.