Ijumaa , 25th Mei , 2018

Nchi wanachama wa mkutano wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wamepitisha azimio la kutambua kuumwa na nyoka kuwa ni suala linalohitaji kupewa kipaumbele katika kulishughulikia.

Maelfu ya watu hufa kila mwaka na wengine kuwa walemavu kutokana na sumu inayotokana na shambulio la nyoka.

WHO imesema athari zinazotokana na kuumwa na nyoka zimeendelea kuwa moja kati ya magonjwa ya kitropiki ambayo hayatiliwi maanani.

Kufikiwa makubaliano hayo kwa nchi wanachama wa WHO, kuna nia ya kuhakikisha kuwa kuna mbinu za kuzuia, kutibu na kukabili mashambulizi ya nyoka.

Kila mwaka zaidi ya watu laki moja hufa duniani kutokana na kuumwa na nyoka huku asilimia 20 wakiwa ni kutoka barani Afrika, ambapo wengine nusu milioni wana ulemavu kutokana, na kukatwa viungo na ulemavu mwingine kutokana na mashambulizi ya nyoka.