Jumatano , 6th Jul , 2022

Halmashauri zilizo na maeneo ya vivutio vya utalii kote nchini zimetakiwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kabla ya kuanzisha tozo mpya kwa watalii wanaotembelea vivutio hivyo ili tozo hizo zisiwe kikwazo kwa watalii wanaokuja nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wilayani Wanging'ombe, wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya uhifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengere.

Waziri Chana ameeleza kuwa jitihada alizofanya na anazoendelea kuzifanya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kuitangaza sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour ni lazima ziungwe mkono na wadau mbalimbali na Halmashauri zote kwa  kuhakikisha zinaweka mazingira mazuri na rafiki kwa watalii.