Jumapili , 25th Jul , 2021

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imezuia mikusanyiko yote isiyokuwa ya lazima ikiwemo ya kidini na siasa, mpaka pale itakapotoa maelekezo mengine na endapo ikihitajika kufanyika mkusanyiko itabidi kitolewe kibali maalum. 

Abiria wakigombania daladala

Agizo hilo limetolewa leo Julai 25, 2021 na Prof. Abel Makubi ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, ambapo amegusa maeneo mbalimbali ikiwemo daladala, misiba, matamasha ya muziki na michezo.

Prof. Makubi amesema, “Misiba yote ibada isizidi dakika 30 mpaka saa 1 na wahudhuriaji wawe wachache, hatujazuia kukaa misibani lakini mzingatie taratibu ikiwemo uvaaji Barakoa, unawaji mikono na kukaa umbali wa mita moja.”

“Daladala zote zipakie ‘Level seat’ isipokuwa zenye nafasi kama mwendokasi abiria wasimame mbalimbali wapeane nafasi huku wakiwa na barakoa, lakini pia Bodaboda haitoruhusiwa kupanda mishikaki”- Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara Afya. 

Ameongeza kuwa idadi ya watakao kwenda kuona wagonjwa hospitali ipungue waruhusiwe ndugu wawili tu asubuhi na wasizidi watatu wodini katika kitanda cha mgonjwa na wengine wawili wataingia jioni au mchana.

Aidha Prof. Makubi amesema, “Mahabusu wote wanaoingia gerezani kwa mara ya kwanza au mtu aliyehukumiwa lazima apimwe kabla ya kuingia gerezani, lakini pia ndugu watakaokwenda kusalimia magerezani ataingia mmoja mmoja”.