Jumapili , 2nd Dec , 2018

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe ameweka wazi ndoto yake ya kugombea Urais na kuahidi kuteua baadhi ya watendaji akiwemo Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Fatma Karume.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe.

Zitto kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter hii leo ameandika kuwa, "Ninaamini nitakuwa Rais bora kwa uwezo wake Mola. Nitauona upinzani kama chachu ya Maendeleo badala ya kuwa na hofu nao. Nitarejesha taswira chanya ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa kwa kulinda Demokrasia na haki za binaadam. Mtachapa kazi, Lakini pia mtakula bata".

Hakuishia hapo, amesema katika uongozi wake, atamteua Fatma Karume ambaye sasa ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kumsaidia kwenye mabadiliko ya mfumo wa utoaji haki nchini.

"Nitamteua kusimamia mabadiliko makubwa ya mfumo wa utoaji haki nchini ili kukomesha vitendo vya uonevu na ukatili. Kwa matendo ya nyuma tutaunda Tume ya Ukweli na Maridhiano ili wahanga wajitokeze kwa uwazi na wahusika wa matendo haya wahukumiwe na umma", amesema Zitto.

Mara kadhaa Zito amekuwa akizungumzia ndoto zake za kushika nafasi ya juu ya kisiasa nchini licha ya kupitia matatizo kadhaa na amekuwa akieleza na kuamini kuwa ataweza kufanikiwa kushika wadhifa huo kama ilivyokuwa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa India, Indira Gandhi.