Ziwa Kisiba na uwepo wa nyoka mwenye vichwa viwili

Jumanne , 10th Sep , 2019

Ziwa masoko au Kisiba linapatikana Mkoani Mbeya katika Wilaya ya Rungwe umbali wa Kilomita 19 kufika eneo hilo ukitokea Tukuyu Mjini.

Ziwa masoko au Kisiba.

Kuna masimulizi mengi kuhusu Ziwa hilo mengi yakiwa ya Kitamaduni zaidi, na hii ndiyo huvutia watu wengi kwenda kutalii. Inaaminika wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia wakati Wajerumani wakiondoshwa walificha masanduku ya mali nyingi za thamani katika Ziwa hilo.

Mpaka sasa inaelezwa mali hizo zipo lakini hakuna ambaye ameweza kuzichukua kwa kile kinachodaiwa uwepo wa nguvu za ajabu pamoja na Nyoka mkubwa mwenye vichwa viwili ambae analinda mali hizo.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Mratibu Mkuu wa Everyday Mbeya, Taasisi inayohusika na kuwatembeza Watalii mbalimbali ndani ya Mkoa huo, Shah Mjanja anasema stori hizo ni masimulizi lakini hakuna uthibitisho wowote wa uwepo wa mali hizo.

"Nimewahi kufanya utafiti kidogo binafsi ni kweli kuna baadhi ya watu wanasema ukiogelea kwenda chini sababu Ziwa lina kina kifupi tu kama mita 70, unaweza kuona masanduku ya kale ambayo yanahusishwa na hiyo ishu ya Wajerumani," alisema.

Aidha simulizi nyingine inaelezea kuwa Ziwa hilo lilitokea ikiwa ni ufunuo aliopata mtu mmoja ambaye inasemekana alitokea Malawi.

Mtu huyo aliomba maji ya kunywa lakini wenyeji wa eneo hilo walimnyima lakini alitokea mtu mmoja ambaye alimpatia maji na ndipo akamwambia mtu aliyempatia maji kuwa aondoke eneo hilo sababu kesho yake eneo zima litatawaliwa na maji, ndiyo chanzo cha Ziwa hilo.

“Kuna Masimulizi mengi kwa mdomo, na kama unavyojua kwa waswahili linalozungumzwa sana huenda lipo lakini sisi hatupo sana huko kwa sababu yanavuruga utalii lakini masimulizi hayo yapo kweli,” aliongeza zaidi.