Jumamosi , 1st Aug , 2020

Zoezi la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kukabidhi ofisi rasmi kwa Mkuu wa Mkoa huo wa sasa Aboubakar Kunenge limesogezwa mbele, hadi siku ya Jumatatu baada ya ratiba hiyo kuingiliana na ratiba zingine.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Taarifa ya kuahirishwa kwa zoezi hilo, imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, ambapo hii leo Agosti Mosi, Makonda alitarajiwa kukabidhi ofisi hiyo iliyopo maeneo ya Ilala, majira ya saa 7:00 mchana.

Makonda aliondolewa kwenye nafasi hiyo siku ya Julai 15, 2020, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, na nafasi hiyo ilichukuliwa na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo.

Machi 13, 2016, Rais Magufuli alimteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo awali kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na hivyo amehudumu kwenye nafasi ya Ukuu wa Mkoa kwa zaidi ya miaka mitatu.