Jumanne , 17th Dec , 2019

Muimbaji wa Nyimbo za Injili hapa nchini Martha Mwaipaja, amesema kuwa japokuwa kuna watu amewavunja Moyo baada ya yeye kuachana na mume wake, lakini yeye hajali kwa sababu anajua magumu aliyokuwa anayapitia na kwa sasa hana maamuzi yoyote juu ya kuolewa au kuwa na mahusiano mapya.

Muimbaji wa nyimbo za Injili, Martha Mwaipaja.

Hayo ameyabainisha leo Disemba 17, 2019, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa kama binadamu haupaswi kuishi maisha yakusikiliza watu, maana ukifuata maneno yao unaweza ukafa kabla ya wakati, huku nyuma ukiacha watoto wako wakiteseka.

"Kuvunjwa Moyo ni kitu tofauti na maisha halisi ya mtu na ukisema uishi kwa sababu ya watu utakufa kabla na utaacha watoto wako wanateseka kwa sababu tu kuna mtu mbele yako, hakuna mtu anajua yale nimekutana nayo,siko kuongelea Ndoa wala mahusiano hivyo vitu ni maamuzi na saa hii sina maamuzi nitajibu kitu gani sasa wakati ndani yangu siko kuongelea hicho"amesema Martha Mwaipaja.

Martha Mwaipaja amesema kuwa kwa sasa anajiona ameshusha mzigo mkubwa ambao umebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa na kwamba yeye na mume wake hawako pamoja kwa muda wa miaka miwili sasa.