Jumanne , 4th Mar , 2014

Msanii mahiri wa filamu hapa Bongo, Ivone Cherrly maarufu zaidi kama Monalisa, amewataka wasanii wa filamu hapa Tanzania kuacha tabia ya kuchukiana na kutokupeana misaada katika kazi zao kwa lengo la kuweza kufikisha sanaa hii ya uingizaji katika ngazi ya kimataifa zaidi.

Msanii huyu amesema kuwa, kuna haja ya kuanza kufikiria kupeleka kazi zao za kisanaa katika ngazi ya kimataifa, na pia kupeana sapoti ya kutosha, akitolea mfano wa msanii Juma Rajab maarufu zaidi kama Cheche Mtungi ambaye yupo katika kinyanganyiro cha tuzo za kimataifa, ambapo amewataka wanasanaa na mashabiki kujitolea kumtangaza na kumpigia kura.

Monalisa amesema kuwa, imefika wakati sasa wasanii kuanza kufikiria kupanua wigo wa kazi zao na kulilenga soko na matamasha na majukwaa ya kimataifa huku kila mmoja akipenda na kusapoti kazi ya mwenzie.

Monalisa ameyasema haya alipokuwa akizungumzia msanii Lupita Nyong'o kutoka Afrika Mashariki ambaye ameweza kupenya hadi kufikia ngazi ya juu kabisa katika uigizaji kwa kushinda tuzo mahiri za filamu za Oscars.