Mr Blue adai kuna wasanii hawana nidhamu

Jumatatu , 7th Oct , 2019

Rapa Mr Blue kupitia mahojiano aliyofanya na EATV & EA Radio Digital, ameeleza kuwa vijana ambao wapo kupitia kundi la “B.O.B Micharazo” wamekuwa wakimkosea heshima kutokana na kauli ambazo wanazitoa kwenye vyombo vya habari.

Mr Blue amesema hayo baada ya kuwepo na taarifa za kuvunjika kwa kundi hilo la muziki na kuwaacha baadhi ya wasanii ambao hawana nidhamu ndani ya kundi hilo.

Wale wote ni vijana wangu, hata ukiangalia stori mimi ndiye niliyewatangaza kwenye muziki ila kilichotokea ni kuwapunguza na kuwaacha baadhi ya wasanii ambao hawana nidhamu, kama binadamu wa kawaida naumia kusikia kauli wanazoziongea, naona vijana wangu wananikosea kinidhamu lakini kukoseana kwenye familia ni jambo la kawaida na tumetoka mbali” amesema Mr Blue.

Aidha amesema kuwa kwa sasa kuna mgogoro wa kibiashara ambao umetokea ndani ya kundi hilo ila tayari ameshawasiliana na msanii Nyandu Tozzy, ambaye kwa pamoja walikuwa wanaliongoza kundi hilo ili kuyamaliza.

Akizungumzia suala la kuachia kazi mpya, Mr Blue ametoa wimbo mpya aliomshirikisha Rich Mavoko na kudai kuwa wimbo huo ndiyo ulimuhitaji zaidi Mavoko, kuliko yeye alivyotaka ashiriki.