Jumatano , 24th Jan , 2018

Msanii wa muziki wa Hip Hop Bongo ambaye alianza game akiwa kinda, Heri Samir au Mr. Blue, ameelezea hisia zake juu ya kukosa tuzo yoyote ya muziki hapa bongo, hata nje ya nchi.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Mr. Blue amesema anaumia sana kuona mpaka sasa hana tuzo yoyote, wakati na yeye ni miongoni mwa rappers wanaofanya vizuri kwenye game.

“Nikiwa nalala na familia yangu naumia sana kuona vile vichuma havipo mezani, na naumia kwa nini hawajanitafutia hata category ya kuniweka, kwenye wasanii wa hip hop mimi huwa siwekwagi, kina Fid wapo, ukija kwenye RnB kina Ben Pol wanawekwa, ila natoa ngoma kali tu, mi mwana hip hop najiona mi nipo tu”, amesema Mr. Blue.

Kutokana na hilo Mr. Blue amesema hivi sasa hataki tena tuzo yoyote ya muziki ya ndani ya Tanzania, labda iwe kutoka nje ya Tanzania kwani ameshakata tamaa.

“Sitaki tena tuzo nimesubiri kwa muda mrefu sana, Tanzania sihitaji tuzo yoyote, nje ya Tanzania poa, yani siwezi kuwa na hamu ya kuitaka tuzo sasa hivi naangalia familia yangu tu”, amesema Mr. Blue.