Msanii wa muziki wa Bongo Flava Timbulo
Timbulo ameweka hayo wazi katika kipindi cha Planet Bongo ambapo amesema mwaka 2011 baada ya kupambana na maisha sana aliamua kuacha ualimu na kujikita kwenye muziki ambapo ngoma ya kwanza ilidunda ngoma ya pili ikawa ‘Domo langu’ ambapo baada ya kuona na yenyewe alikoipeleka ili ichezwe kwenye redio haipewi nafasi wala kusikika akaamua kurudi nyumbani Mbeya.
‘’Kuna mtu mmoja yupo kwenye kituo cha redio nilimpelekea ngoma yangu ila kila nilipokuwa nikimpigia simu akawa hapokei simu yangu akawa ananizungusha hadi nikakata tamaa nikaaamua kurudi nyumbani kwenda kujikita kwenye kilimo nyumbani Mbeya’’ Amesema Timbulo.
‘’Nilianza kulima baada ya miezi miwili yule mdau akanipigia simu akaniambia ngoma yangu ni nzuri na itanifikisha mbali, nikamwambia mama yangu, mama yangu akaenda kukopa shilingi elfu 30 ambayo ilikuwa inatosha kupanda basi hadi Dar es salaam nikabeba zangu ndoo moja ya maharage na moja ya mchele kuja kuanza maisha mapya, baada ya kufika kweli ngoma ya ‘Domo langu ikawa ni kitu kingine ikanitambulisha kwenye tasnia’’ Amesisitiza Timbulo.
Aidha Timbulo amesema kwamba mama yake amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anafanikiwa katika tasnia ya muziki jambo ambalo limepelekea yeye pia kufika hapo alipo.






