Jumamosi , 3rd Sep , 2016

Jaji wa mashindano ya Dance100% kwa mara 5 mfulilizo Super Nyamwela leo ametoa alama 100% kwa mara ya kwanza tangu aanze kuwa jaji wa mashindano hayo ,kutokana na uwezo wa kutisha wa kundi la J. Combat Crew kutoka Zanzibar.

Akizungumza na EATV mara baada ya kumalizika kwa hatua ya nusu fainali, Jaji Nyamwela amesema ameamua kutoa alama hizo kutokana na ubunifu wa hali ya juu wa washiriki hao, ambapo wameweza kuonesha kiwango ambacho hakijawahi kuoneshwa na wengine tanguu aanze kuwa Jaji wa shindano hilo.

“J. Combat kiukweli wameniridhisha , kutokana na kiwango walichoonesha katika raundi ya pili ya mchuano wa leo, wamebainisha wazi kwamba wapo vizuri na wamechukulia mashindano hayo kwa umakini wa hali ya juu ndiyo maana nimewapa alama hizo na kila mtu ambaye ameshuhudia kiwango cha leo amefurahishwa na namna walivyokuwa wabunifu” Amesema Jaji Nyamwela.

Aidha Nyamwela ameongeza kuwa ili kundi liweze kujihakikishia ushindi ni lazima, kama ni nyimbo mbili zote wazifanyie haki ili wafaidi alama za awamu zote, na kubainisha kwamba kundi hilo la J Combat wamefanya vizuri sana awamu ya pili ila awamu ya kwanza hawakufanya vizuri jambo ambalo limefanya wasipate alama nyingi za kutosha na kutinga fainali.

Kundi hilo la J Combat kutoka Zanzibar limeshindwa kuendelea na shindano hilo kutokana na alama za mjumuisho kutotosha baada ya wimbo wa kwanza kuonekaa kufanya vibaya ikilinganishwa na wimbo wa pili ambao wameonekana kufanya vizuri zaidi.

Shindano la Dance100% linaendeshwa na EATV na kudhaminiwa na Vodacom pamoja na Coca Cola na kurushwa na EATV siku ya Jumapili kuanzia saa moja jioni.

Tags: