Steve Nyerere amvaa tena Peter Msigwa

Ijumaa , 7th Feb , 2020

Msanii maarufu wa filamu hapa nchini Steve Nyerere, ametangaza nia yake ya kugombea Ubunge katika jimbo la Iringa mjini baada ya kupokea maombi mbalimbali kutoka kwa vijana wenziye pamoja na marafiki.

Kushoto pichani ni msanii wa filamu Steve Nyerere, kulia ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa

Steve Nyerere ametangaza nia yake hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, ambapo ameandika.

"Iringa ya leo ni maendeleo kwanza na inahitaji vijana wachapakazi, rasmi nitagombea Ubunge Iringa Mjini ni haki yangu kurudi nyumbani, siku ya Jumatano nitakuwa na kikao cha ndani na vijana wa Iringa ahsante" amesema Steve Nyerere.

EATV & EA Radio Digital, imefanya mawasiliano na msanii huyo wa filamu na ameeleza kwa kina kwa nini ameamua kugombania Ubunge Iringa Mjini ambapo amesema,

"Nina dhamira ya kweli ya kugombania Ubunge katika Mkoa wangu, naijua vizuri Iringa kuliko watu walivyoisoma, hatutaki tena kuwatuma watumishi wazee ambao wanatafuta pesa ya pensheni, tunataka vijana wenye kuijua Iringa na lazima wanitume mtu kama mimi" amesema Steve Nyerere.

Pia ameendelea kusema "Mimi ni mkubwa najulikana nchi nzima na Afrika Mashariki yote, huwezi kunifananisha na Peter Msigwa anayejulikana mwisho Tosamaganga na Mahenge, nina uwezo na juhudi, labda aje kuniomba msamaha na anatapatapa anataka kushindana na watu na wake za watu atarudi kwenye Uchungaji".