Ijumaa , 16th Dec , 2016

Meneja wa wasanii Petit Man ambaye hivi karibuni alikutwa na balaa la kukimbiwa na msanii wake akidai anamtumia kuingiza pesa, amesema wasanii wengi hudharau mameneja na matokeo yake huishia kubaya.

Petit Man

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Petit Man amesema hapo awali tatizo hilo lilikuwa linampa wakati mgumu, lakini kwa sasa ameshawazoea wasanii hivyo halimsubui kichwa tena.

"Changamoto ni nyingi sana ambazo nakutana nazo, ila nishazizoea tu lakini mwanzo ndio zilikuwa zinanipelekesha sana, lakini saa hivi kitu chochote kikitokea mi naona cha kawaida tu, kwa sababu wasanii wanakuwa wananidharau, wanaongea lakini mwisho wa siku muendeleo wao unakuwa siyo mzuri wanaishia tu kupotea, kwa hiyo mi kazi yangu niliyokuwa nafanya inaonekana hapo", alisema Pet man.

Petit Man aliyendelea kwa kusema kuwa msanii yeyote anahitaji usimamizi, ili awe na muda wa kutosha wa kufanya kazi nzuri, huku masuala mengine yakifanywa na uongozi wake. 

"Muziki mzuri unatakiwa kuwa na menejimenti iwe inasimamia, msanii kazi yake ni kuimba tu vitu vingine iachie menejimenti, msanii akikosa menejimenti ndiyo chanzo cha kupotea", alisema Petit Man.