Alhamisi , 21st Apr , 2016

Mbunge wa Kasulu Mjini Mkoani Kigoma Mhe. Daniel Nswanzingwanko (CCM) amesema kwamba ili msanii awe mzuri lazima awe na asili ya Mkoa wa Kigoma.

Mbunge wa Kasulu Mjini Daniel Nswanzingwanko (Picha ya Maktaba)

Mhe. Nswanzingwanko ameyasema hayo alipokuwa akiuliza swali katika bunge la 11 kikao cha tatu kuhusu ni lini serikali itajenga chuo cha sanaa mkoani Kigoma ili kukuza zaidi vipaji vya wasanii wengine.

''Kuna wasanii wengi wenye asili ya Kigoma kama Diamond, Ali Kiba, Mrisho Mpoto na wengine wengi na huwezi kuwa msanii mzuri kama huna asili ya Kigoma,'' alisema Mbunge Nswanzingwanko.

Akijibu swali la Mbunge huyo Naibu Waziri Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi. Anastazia James Wambura amesema serikali inathamini mchango wa wasanii wote nchini na kuzitaka halmashauri zote nchini kuajiri maafisa utamaduni ili kuhakikisha wanashughulikia masuala ya wasanii kwa ukaribu zaidi.