Wastara
Wastara ameeleza hayo alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv baada ya kuwepo kwa tetesi kutoka mitandaoni pamoja na kwa mashabiki zake kuwa huenda mwanamama huyo ameshindwa kuendelea kuigiza kwasababu ya kuumwa mara kwa mara.
"Naendelea kufanya kazi zangu kama kawaida na kuhusu suala sanaa ni kwamba sijaamua kuacha katika kipindi hiki endapo nitaamua kufanya hivyo nitasema, ila kwa sasa ninaweka vizuri viungo vyangu na vitu vingine kutokana na takribani miaka mitatu sikufanya kazi 'serious'.....
Vitu vingi sana katika maisha yangu vimeenda ndivyo sivyo kwa hiyo nipo kama mtu ambaye anaanza upya maisha na ndio maana inanibidi nijiweke sawa kutokana mimi ni mama mwenye majukumu", amesema Wastara.
Pamoja na hayo, Wastara ameendelea kwa kusema "kuugua siyo kitu cha siku moja kwamba umeenda hospitali umerudi na ujiite wewe ni mzima. Nafikiri tumeona hata yale aliyoyapitia marehemu mzee Majuto kuwa aliumwa alipelekwa hospitali lakini akawa bado mgonjwa, hali kadharika nami nipo hivyo hivyo".
Wastara ni miongoni mwa wasanii wanaopitia maisha magumu kutokana na maradhi yake yanayomsumbua ya mgongo na kichwa ambayo yamesababishwa na ajali aliyoipata miaka ya nyuma na kusababisha kupoteza mguu wake mmoja .
Mwanzoni mwa mwaka huu hali ya Wastara ilikuwa mbaya zaidi hali iliyolazimu watu mbalimbali na viongozi kutoka serikali kuu kumchangia takribani Shilingi milioni 18,ili kwenda nchini India kupatiwa matibabu ya mguu wake ambao ulikuwa una maumivu makali hadi muda mwingine kupoteza fahamu.





.jpg?itok=XbSGwlDp)

