"Walisema natupa pesa" – Paul Makonda

Ijumaa , 7th Jun , 2019

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa uponyaji wa Pascal na kumpa moyo wa kusimama naye, japo watu wengi walimkatisha tamaa.

Paul Makonda ameyasema hayo mara baada ya kuonana na mwanamuziki huyo wa Injili Pascal Kasian, alipokwenda kumsalimia ofisini kwake, baada ya kurudi kutoka India ambako alikuwa amekwenda kutibiwa.

“Wako watu walikuwa wananufaika na ugonjwa wake, baadhi ya watu walisema hawezi kupona na wengine kusema hadharani kuwa pesa nilizotoa kwaajili ya matibabu ni sawa na kutupa pesa kwenye shimo la choo, yalikuwepo kila aina ya maneno ya kukatisha tamaa, lakini leo amerudi na kusema imewezekana”, amesema Paul Makonda.

Naye Pascal Cassian amemshukuru Paul Makonda na kumhakikishia kuwa amepona na sasa anaweza kuendelea na shughuli zake za kutafuta kipato kama alivyokuwa awali.

Ikumbukwe kwamba Paul Makonda alitoa ahadi ya kugharamia matibabu yake ndani na nje ya nchi na hivi karibuni alimpatia kitita cha fedha kwaajili ya Matibabu nchini India, Tiketi ya Ndege kwa watu watatu waliomsindikiza pamoja na fedha ya malazi kwa siku zote walizokuwa wakipata matibabu Nchini India.