Jumatano , 28th Dec , 2022

Musa Hasahya ni mkulima kutoka Butaleja nchini Uganda ambaye ana wake 12, watoto 102 na wajukuu 568 amesema kwamba hatoongeza tena ukubwa wa familia yake kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Musa akiwa na watoto wake

Musa ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuwataka wake zake kuanza kutumia uzazi wa mpango ili familia iweze kununua mahitaji ya chakula yatakayokidhi familia.

"Kipato changu kimekuwa kikishuka chini kutokana na kupanda kwa gharama za maisha na familia yangu imekuwa kubwa na kubwa zaidi, nilioa mwanamke mmoja baada ya mwingine, mwanaume anawezaje kuridhika na mwanamke mmoja," amesema Musa

Kuoa wake wengi ni halali nchini Uganda, lakini wake zake wote wanakaa kwenye nyumba moja ili kuwazuia wasiweze kutoroka na wanaume wengine.

Aidha Musa hawezi tena kufanya kazi kwa sababu ya afya yake kuzorota kutokana na maradhi na wake zake wawili wameondoka kutokana na changamoto za kifedha.

Zulaika, mke wake mdogo na mama wa watoto wake 11, amesema, "Sina watoto tena, nimeona hali mbaya ya kifedha na sasa natumia tembe (vidonge) ya kupanga uzazi, Lakini dawa za kupanga uzazi ni mwiko nchini, kwani mara nyingi zinahusishwa na uasherati,".

Umri wa watoto wa Musa ni kati ya miaka sita hadi 51, na takriban theluthi moja ya watoto wake wanaishi na Musa nyumbani kwake.