Rose Muhando alivyokataa kutumikishwa kingono

Jumamosi , 19th Oct , 2019

Msanii wa nyimbo za Injili nchini Tanzania Rose Mhando, ameeleza jinsi alivyotakwa kimapenzi na meneja wake kipindi alipokuwa na matatizo ya afya, pamoja na kudaiwa kutumia madawa ya kulevya na kuabudu mashetani.

Rose Muhando

Rose Muhando ameeleza hayo katika mahojiano na kituo cha habari nchini Kenya, ambapo amesema taarifa za yeye kutumia madawa ya kulevya na kuabudu mashetani ni za uongo na zilisambazwa na aliyekuwa meneja wake baada ya kumkatalia kufanya naye mapenzi.

"Aliyekuwa Meneja wangu aliamua kunipangia kashfa kwa nia ya kuharibu jina langu, sikutaka kuwa mtumwa wa ngono, sitaki hata leo potelea mbali, hata kama yeye alitaka kuchukua vitu vyangu, akaamua kunitengenezea kashfa sababu nilimkataa basi na iwe hivyo lakini Mungu akibaki na mimi peke yake inatosha, maana yeye anajua hesabu za siku zangu" amesema Rose Muhando.

"Kwani mara ngapi nimechukuliwa nikapelekwa milimani, nikapelekwa msituni na kuwekewa bastola kichwani nikubaliane na kile ambacho sitaweza kulisema lakini nilikataa nikasema niko radhi kufa hata kwa dakika moja, siwezi kukubaliana na utumwa ambao walitaka kunitumikisha nao" ameongeza.

Pia amemshukuru Mchungaji maarufu nchini Kenya aitwaye Pastor Ng'ang'a kwa kumfanyia maombi na kumponya matatizo yake.