"Sio kitu rahisi kuwa na mimi" - Posh Queen

Jumatano , 12th Dec , 2018

Mlimbwende maarufu nchini Tanzania hasa katika mitandao ya kijamii, Jacline Obedi maarufu kama 'Posh Queen', ameweka wazi kuwa ni vigumu kwa wanaume kummiliki, licha ya kuwa na urembo wa kumvutia kila mmoja.

Akizungumza na Big Chawa kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Posh ameweka wazi kuwa yeye sio mdangaji kama ilivyo kwa wadada wengi wa mjini, kwani anajihudumia mwenyewe, hivyo ni vigumu kwa mwanaume kumpata kirahisi kwa sababu ya pesa, kwani mwenyewe anajua kutafuta pesa na anajihudumia.

“Sio kitu rahisi kuwa na mimi unatakiwa ujue, sio mtu ambaye nitachukua vitu vyako, au nini, mimi najihudumia, isipokuwa kama mwanaume wangu unatakiwa uwajibike lakini sio kama mimi siwezi kujihudumia, kuanzia miamala, uwe na akili timamu”, amesema Posh.

Pia Posh ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu katika masuala ya kuthibiti majanga, amesema kwamba anaingiza mkwanja mrefu unaotokana na biashara yake ya mikanda.