Jumamosi , 17th Nov , 2018

Uongozi wa jamii ya Kwazulu Natal huko Afrika Kusini, imewataka wanaume ambao wana umri wa kuoa kulipa kodi, na kuwa na barua ya utambulisho wa umiliki wa makazi.

Kwenye taarifa ambayo imeripotiwa na vyombo mbali mbali vya habari nchini humo, imeeleza kwamba kodi hiyo ambayo inagharimu Randi 50 ya Afrika Kusini ambayo ni sawa na zaidi ya shilingi 8,200 za Tanzania, wanatakiwa kulipa kila mwezi.

Kitendo hicho kimeanza kulalamikiwa na watu wengi wakiwemo wazazi wa vijana ambao hawajaoa na hawana kazi, kwani wao ndio hulazimika kuwalipia kodi hizo.

Mmoja wa wazazi hao Busisiwe Mthembu, amenukuliwa akisema “Wanalipa kodi, ingawa hawajaoa, nililipa kwa kijana wangu wa kwanza, na wapili akafika miaka 18, nikapaswa kumtafutia barua ya umiliki wa makazi na kulipa, wa tatu ambaye naye anaingia miaka 18 naye hajaoa na yuko Johanesburg anatafuta kazi”.

Kiongozi wa eneo hilo Thathezakhe Ngobese, amesema kwamba kodi hiyo siyo kwa ajili ya kulisha familia yake, bali hutumika kusaidia matumizi madogomadogo kwenye uongozi wao ikiwemo mahakama za kijamii, wanaofanya usafi maeneo hayo na mengineyo.