1. Michael Scott (1977–1981)
Katika miaka ya mwanzo, wawekezaji walihisi kuwa vijana akina Steve Jobs walihitaji "msimamizi wa watu wazima." Michael Scott akawa CEO wa kwanza. Alikuwa mtu wa nidhamu na ndiye aliyeweka misingi ya kwanza ya kibiashara wakati Apple II ikianza kutamba.
2. Mike Markkula (1981–1983)
Markkula hakuwa kiongozi tu; alikuwa mwekezaji mkubwa aliyetoa mtaji wa kwanza. Alichukua usukani kwa muda mfupi akiamini kuwa Apple inaweza kuwa kampuni ya kibiashara ya kudumu, si hobby ya vijana tu.
3. John Sculley (1983–1993)
Huyu ndiye mtu Steve Jobs aliyemshawishi kwa swali maarufu: "Je, unataka kuuza maji ya sukari maisha yako yote, au unataka kuja nami tubadilishe dunia?" Sculley alikuja kutoka Pepsi, lakini baada ya muda, yeye na Jobs walitofautiana vibaya, hali iliyopelekea Steve Jobs kufukuzwa kwenye kampuni yake mwenyewe.
4. Michael Spindler (1993–1996)
Spindler alipewa jina la utani "The Diesel" kwa sababu ya kufanya kazi kwa nguvu kubwa. Aliongoza wakati wa mpito mgumu wa kwenda kwenye vichakata vya PowerPC, lakini kampuni ilianza kuyumba kiuchumi chini ya uongozi wake.
5. Gil Amelio (1996–1997)
Ingawa alidumu kwa muda mfupi zaidi, Amelio alifanya maamuzi ya kihistoria: Kuinunua kampuni ya NeXT. Kupitia ununuzi huu, hakupata tu mfumo mpya wa uendeshaji (OS), bali alimrudisha Steve Jobs nyumbani.
6. Steve Jobs (1997–2011)
Hii ndiyo enzi dhahabu. Jobs alirudi na kuifuta Apple kwenye ukingo wa kufilisika. Alitupa bidhaa zilizobadilisha maisha yetu: iMac, iPod, iPhone, na iPad. Alikuwa kiongozi mwenye maono makali aliyewafanya watu wapende teknolojia kama sanaa.
7. Tim Cook (2011–2026)
Baada ya Jobs kufariki, wengi walitabiri anguko la Apple. Lakini Tim Cook alithibitisha kinyume chake. Aliifanya Apple kuwa kampuni yenye thamani kubwa zaidi duniani, akijikita kwenye huduma (Services), Apple Watch, na AirPods. Chini yake, Apple imekuwa ngome ya kiuchumi duniani kote.
8. John Ternus (Kuanzia Septemba 1, 2026)
Sasa, tuko kwenye kizingiti cha historia mpya. Kuanzia Septemba mwaka huu, John Ternus, ambaye amekuwa kiongozi wa uhandisi wa vifaa (Hardware Engineering), anapokea kijiti. Ulimwengu unasubiri kuona jinsi "damu changa" hii itakavyoendeleza ubunifu kwenye enzi ya Akili Bandia (AI) na vifaa vya kisasa zaidi.




