Jumanne , 14th Aug , 2018

Afisa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema waliamua kutowafunga Namungo FC ili kuweka heshima kutokana mwaliko wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kwenda nayo suluhu ya 0-0.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na wachezaji wa Simba.

Simba walikuwa na mchezo wa kirafiki siku mbili zilizopita dhidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza kwa ajili ya uzinduzi wa Uwanja wa Majaliwa uliopo mjini Ruangwa, Majaliwa aliwaalika Simba ili wakacheze na Namungo kwa ajili ya uzinduzi hivyo Manara ameeleza ilibidi watumie busasara ili wasiweze kuleta aibu kwa Waziri.

"Tuliamua kutowafunga Namungo kwa ajili ya heshima ya Waziri, hauwezi kumwaibisha mtu mkubwa kama yule mwenye heshima zake" amesema.

Katika hatua nyingine klabu hiyo imewasili jana jioni jijini Arusha baada ya kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa huo, Mrisho Gambo ambaye amewaalika Simba kwa ajili ya kucheza na Arusha United ambayo ilikuwa inajuliakana kama JKT Oljoro iliyopo Ligi Daraja la Kwanza.

Kikosi cha Simba kitautumia mchezo huo kama maandalizi kuelekea mechi dhidi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa Agosti 18 kwenye Uwanja wa CCm Kirumba, Mwanza.