Alichokisema Senzo kuhusu kujiuzulu kwake

Jumapili , 9th Aug , 2020

Klabu ya soka ya Simba imepata pigo kufuatia Mtendaji wake Mkuu, Senzo Mbatha kujiuzulu nafasi yake hii leo.

Senzo Mbatha na Haji Manara

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter, Senzo ameandika ujumbe wa kuushukuru uongozi wa klabu hiyo kwa nafasi ambayo umempa kuiongoza klabu na kujivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi.

Senzo alijiunga mwaka uliopita ndani ya klabu hiyo na kujizolea sifa nyingi za kiuongozi pamoja na kuisaidia klabu kushinda mataji matatu msimu wa 2019/20 ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu Tanzania bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Pia katika msimu wake wa kwanza, Simba ilifanikiwa kuvuka hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kufanya  vizuri katika michezo ya kundi lake.