Jumamosi , 9th Nov , 2019

Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Aussems ameitaja sababu ya kutowachezesha wachezaji Miraji Athumani na Mzamiru Yassin katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons uliopigwa Alhamisi ya wiki hii.

Kocha Patrick Aussems, Mzamiru Yassin na Miraj Athumani

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa taifa, Simba ililazimishwa sare ya kutofungana na Tanzania Prisons, ambapo baada ya mchezo mashabiki wa Simba walionekana kulalamikia juu ya sababu za kutowapanga wachezaji hao.

Akizungumza katika mazoezi ya timu Ijumaa, Novemba 8, kocha Aussems amesema kuwa alimpumzisha Mzamiru Yassin baada ya Jonas Mkude kurejea kikosi cha kwanza na ambaye anaimudu vizuri namba hiyo, huku akitaja sababu ya kutompanga Miraji ni kutokana na majeraha.

"Mechi ipo tarehe 24 kwahiyo tuna muda wa kujiandaa, unajua Miraji aliumia hivyo asingeweza kucheza kama ilivyo kwa Bocco na Da Silva.", amesema Aussems.

"Mzamiru hakucheza kwa sababu Jonas Mkude amerudi na tulimbadilisha kwa sababu amecheza mechi zote hizo tano.", ameongeza.

Pia kocha Aussems ametoa siku 2 za mapumziko kwa wachezaji wake, ambapo watarejea Jumatatu, Novemba 11 tayari kujiandaa na mchezo unaofuata wa ligi utakaopigwa Novemba 24, baada ya mapumziko kupisha michezo ya kalenda ya FIFA.