Jumatatu , 6th Jun , 2016

Chama cha Mieleka nchini AWATA kimeshindwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 15 ili kuweza kugomboa vifaa vya michezo vilivyokwama bandarini jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa AWATA Vicent Magessa amesema, wamepokea barua kutoka baraza la michezo nchini BMT ikiwataka kuhakikisha wanakuwa na uwanja wao kitu ambacho hakiwezekani kwa kuwa vifaa vya uwanjani vimekwama bandarini.

Magessa amesema, vifaa hivyo vinatakiwa kuwepo uwanjani na waliomba kusaidiwa lakini bado mpaka leo hakuna jambo lolote lililofanyika ili vifaa hivyo viweze kutolea bandarini.

Magessa ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Michezo kuwasaidi kutoa vifaa vyao bandarini ili waweze kuwa na uwanja wao.

Vifaa hivyo vilitolewa na Shirikisho la Mieleka Duniani (UWW) ambapo viliwasili Aprili mwaka huu lakini hadi sasa vimeshindwa kuwafikia awata kutokana na kutokuwa na fedha kwa ajili ya kulipia kodi.