Jumamosi , 1st Jun , 2019

Klabu ya soka ya Azam FC imetwaa kombe la shirikisho nchini (ASFC), kwa kuifunga Lipuli FC goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa leo kwenye uwanja wa Ilulu mkoani.

Wachezaji wa Azam FC wakishangilia goli

Kombe hilo ambalo limefanyika kwa msimu wa nne sasa tangu kurejea kwake msimu wa 2015/16, halijawahi kuchukuliwa na timu moja mara mbili ambapo kila mwaka fainali imekuwa ikihusisha timu tofauti.

Kwa ushindi wa leo rasmi Azam FC imekata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ambao itaungana na Simba SC ambao wao wametwaa ubingwa wa soka Tanzania Bara na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Goli pekee la Azam FC katika mchezo wa fainali lilifungwa na Obrey Chirwa dakika ya 65 hivyo kuwapa kombe Azam FC ambalo walilikosa mwaka 2015 kwa kufungwa na Yanga kwenye fainali.

Kwenye ligi Azam FC walimaliza katika nafasi ya 3 huku Lipuli FC wakimaliza katika nafasi ya 4 ambayo ni mafanikio makubwa kwao wakiwa katika msimu wao wa pili kwenye ligi tangu waliporejea mwaka 2017.