Jumatano , 9th Jan , 2019

Farid Mussa, Shaaban Idd, Himid Mao ‘Ninja’ na Yahya Zayd ni wachezaji wanaoipa jeuri Azam FC kuwa miongoni mwa klabu iliyofanya vizuri kwenye kutoa vipaji na kuvipeka kimataifa katika miaka ya hivi karibuni tofauti klabu kongwe Simba na Yanga.

Yahya Zayd

Klabu hiyo imekuwa mfano kwenye suala la biashara ya wachezaji ambapo wengi iliwaruhusu wakati ambao inawahitaji zaidi mfano ikiwa ni Shaaban Idd ambaye aliondoka akiwa mfungaji bora wa timu kwenye michuano ya Sportpesa.

Hivi karibuni Yahya Zayd aliondoka nchini kwenda Misri kufanyiwa vipimo vya afya na klabu ya Ismaily ambapo leo Azam FC imethibitisha kufikia makubaliano na klabu hiyo juu ya mauzo ya mshambuliaji huyo chipukizi.

Zayd mwenye miaka 20, yupo nchini Misri tayari hivi sasa kwa vigogo hao wa soka walioingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, ambapo ameshamaliza taratibu zote za kimkataba.

Zayd alikulia kwenye malezi ya soka ya Azam Academy na kupandishwa timu kubwa ya Azam FC msimu uliopita (2017-2018).

Farid Mussa na Shaaban Idd wanaokipiga CD Tenerife ya Hispania, nahodha wa zamani, Himid Mao ‘Ninja’, anakipiga Petrojet ya nchini Misri na sasa ameungana kwenye ligi moja na Yahya Zayd.

Mara ya mwisho mchezaji wa Yanga kwenda nje ni Hassan Kessy aliyekwenda Nkana FC ya Zambia akitanguliwa na Simon Msuva aliyekwenda Morocco huku mchezaji wa Simba akiwa ni Abdi Banda aliyekwenda Baroka FC ya Afrika Kusini.