Jumanne , 6th Dec , 2016

Nahodha wa Klabu ya Azam FC John Bocco ‘Adebayor’ amesema anaamini kikosi hicho kitakuwa vizuri na kukaa nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara

Azam FC wakiwa mazoezini

.

Bocco amesema, morali waliyokuwa nayo wachezaji pamoja na nguvu za nyota wapya walioongezwa kikosini kwenye usajili huu wa dirisha dogo, utaweza kuwasaidia kufanya vizuri.

“Tumeweza kufika na kufanya mazoezi salama kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili, mazoezi tumeanza vizuri, wachezaji wote wana morali, wamerudi wameonekana hawakwenda nyumbani tu kupumzika bali walikuwa wakifanya baadhi ya mazoezi, kwa hiyo naamini mzunguko wa pili utakuwa ni mzuri sana kwetu,” amesema Bocco.

Benchi la Ufundi la Azam FC kwa kushirikiana na uongozi wa timu hiyo, katika usajili huu wa dirisha dogo unaoendelea umeweza kuongeza nguvu mpya kwa kuwasajili washambuliaji nyota wawili kutoka Ghana, Yahaya Mohamed anayetokea Aduana Stars na staa wa Sekondi Hasaacas na Samuel Afful

Pia imewarudisha kundini wachezaji wake wawili waliokuwa kwa mkopo, beki wa kati kinda Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda na winga wa kushoto Enock Atta Agyei (Medeama).

Azam FC mpaka inamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia pointi 35 na Yanga ikiwa na pointi 33.