Azam wababe Mapinduzi Cup, Simba kuifuata Yanga?

Ijumaa , 10th Jan , 2020

Huenda ikawa Azam FC ana ngome yake katika visiwa vya Zanzibar hasa inapokutana na vigogo wa Tanzania bara, Simba na yanga.

Mchezo wa Simba na Azam FC

Mchezo wa leo ni wa tano kuzikutanisha Azam FC na Simba katika michuano ya Mapinduzi ndani ya miaka saba ya karibuni, ambapo mara zote Azam FC imeibuka na ushindi kwa kuiondoa Simba. Mchezo wa kwanza Januari 2012, Azam iliichapa Simba katika Nusu Fainali kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Kipre Tcheche na John Bocco.

Mchezo wa pili uliochezwa mwaka 2016, Azam FC ilikutana na Simba katika Nusu Fainali na kutoka sare ya mabao 2-2 na kisha Azam FC kwenda fainali kwenye mikwaju ya penalti. Mwaka 2017 Azam FC iliifunga Simba bao 1-0 katika fainali na mwaka 2019 pia Simba ikafungwa mabao 2-1 katika Nusu Fainali.

Katika miaka hiyo minne iliyokutana na Simba, Azam FC imefanikiwa kubeba ubingwa mara zote nne. Je, Simba itakubali kuwa mteja wa Azam FC kwa mara ya tano au itapindua meza hii leo?.