Jumatano , 22nd Mar , 2017

Klabu ya Azam FC imesema, wanasubiri ripoti ya Kamishana wa mchezo wao wa marudiano wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows juu ya vurugu zilizotokea katika mchezo huo uliopigwa Machi 19 Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, nchini Swaziland

Kikosi cha Azam FC

Afisa habari wa Azam FC Jaffary Iddy Maganga amesema, wameamua kumuachia kamishina wa mchezo kila kitu kwani yeye alishuhudia vurugu zote zilizotokea kabla ya mchezo huo.

Amesema Kamishna aliruhusu wachezaji wa Azam FC kubadilishia nguo ndani ya gari mara baada ya kujiridhisha na hali iliyokuwa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.

"Tulianza kufanyiwa vurugu mpaka kufikia mtendaji wetu Mkuu Saad Kawemba kupigwa lakini kamishina wa mchezo aliweza kushuhudia kila kitu na hata wakati wa kubadilisha nguo tulikagua kwanza vyumba na tukakutana na harufu ya madawa ambayo kiukweli ukivuta mwili unaisha nguvu. Tulimuambia kamishina ambaye aliingia ndani ya chumba na kujiridhisha na ndipo alipoturuhusu tubadilishie nguo kwenye gari na ukaguzi tufanyiwe tukiwa nje ya vyumba," amesema Maganga.

Maganga amesema, mbali na matukio hayo waliweza kukubali matokeo ya mchezo huo ambao walifungwa mabao 3-0 na kutolewa katika mashindano hayo.

Kikosi cha Azam FC kinaingia kambini hapo kesho kwaajili ya kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga utakaopigwa Aprili mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.