Ijumaa , 24th Mei , 2019

Stori ya mjini hivi sasa si matokeo ya mchezo wa Sevilla na Simba, ila stori kubwa ni namna gani mchezo huo ulivyomalizika hasa baada ya wachezaji wa Simba kuomba 'fair play' kwa wachezaji wa Sevilla.

Salamba na benchi la ufundi la Simba

Stori imekuwa kubwa baada ya mchezaji wa Simba, Adam Salamba kuomba kiatu cha mchezaji wa Sevilla, Ever Banega, huku mashabiki wakionekana kukosoa hatua hiyo kwa hoja dhaifu kuwa amejidhalilisha mwenyewe na klabu yake.

Tukio liliyowahi kutokea mchezaji kuomba kiatu cha mchezaji mwenzake.

Inawezekana ni uelewa mdogo au ni ushabiki uliopitiliza uhalisia, ambao mashabiki wengi wa soka nchini wako nao katika suala hili. Itakukumbukwa katika mchezo wa Raja Casablanca na Atletico Mineiro kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vilabu mwaka 2013, ambapo wachezaji wa Raja Casablanca waligombania viatu vya Ronaldinho Gaucho.

Klabu ndogo inapokutana na klabu ya daraja la juu yake, ni suala la kawaida kwa wachezaji wadogo kuomba jezi, picha na hata viatu kama kumbukumbu kwao kwa sababu wao ni kama vioo vya mafanikio na ndoto ya wanapotaka kufika. 

Pia ni ngumu kwa mchezaji kama Salamba kutegemea kuwa atakuja kukutana na Banega tena kwenye maisha yake ya soka, kwahiyo ni kawaida kufanya vile alivyofanya.

Kutokana na utofauti wa ubora wa wachezaji, Salamba ni mchezaji mdogo sana kwa Ever Banega, ambaye tayari ana medali ya michuano mikubwa barani Ulaya ya Europa League. Kwake ni kama kumbukumbu kuwa na kiatu cha mchezaji huyo.

Kwa kumalizia, klabu nyingi za Kiafrika, pamoja na Tanzania, zina changamoto ya kuwa na wataalamu wa saikolojia za wachezaji. Mfano katika suala kama hili la Salamba, kulitakiwa kuwepo na mtaalamu ambaye angekaa na Salamba na kumwelezea mazingira kama hayo ni ya kawaida katika mchezo hivyo asiyumbishwe na maneno ya watu.