Jumanne , 1st Jan , 2019

Aliyekuwa Kocha wa Mbao FC ya Jijini Mwanza, Amri Said leo ametambulishwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa Biashara United ya mkoani Mara.

Kocha mpya wa Biashara United, Amri Said akisaini mkataba

Amri Said amesaini mkataba wa miezi sita (6) kuitumikia klabu hiyo hadi mwisho wa msimu huu.

Anachukua nafasi ya Hitimana Thierry ambaye hivi karibuni alivunja mkataba na timu hiyo kutokana na mfululizo wa matokeo mabovu yaliyoikumba tangu mwanzo wa msimu.

Kocha huyo mpya wa Biashara United aliondoka Mbao FC kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na uongozi wa klabu baada ya kumtambulisha kocha mpya bila majadiliano naye.

Biashara United imekuwa na matokeo mabaya tangu kuanza kwa msimu huu, ambapo mpaka sasa imeshacheza michezo 17 na kuvuna alama 10 pekee, huku ikishika mkia katika nafasi ya mwisho ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara. Ujio wa kocha huyo unaweza kuwa dawa ya kuipa matokeo mazuri timu hiyo kutokana na kufanya vizuri alipokuwa na Mbao FC.