Ijumaa , 9th Jan , 2015

Baraza la Michezo nchini BMT limesema, limepokea barua kutoka kwa vyama mbalimbali vya tenisi nchini kuhusiana na migogoro iliyopo baina ya vyama hivyo na Chama cha Tenisi nchini TTA.

Akizungumza na East africa Radio, Katibu Mkuu wa BMT, Henry Lihaya amesema, baada ya kupokea barua hiyo waliamua kuandika barua ya majibu ya malalamiko hayo kwenda kwa Katibu mkuu wa TTA ambapo aliombwa kujibu barua hiyo mpaka Januari saba mwaka huu.

Lihaya amesema, mpaka sasa bado hawajapokea barua kutoka TTA, hivyo wanatarajia kukutana na wanachamna pamoja na wadau wa mchezo wa Tenisi ili kuweza kujadili suala hilo.

Lihaya amesema, katika mkutano huo wanatarajia pia kuwaita viongozi wa TTA ambapo kama hatofika, watajadiliana na wanachama na watatoa maamuzi nini kifanyike ili kuokoa chama hicho.