Jumatatu , 1st Dec , 2025

Mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich, Max Eberl, ameatoa taarifa ya kutatanisha kuhusu mustakabali wa Harry Kane, akisema mshambuliaji huyo “anajua kabisa anachotaka”.

Harry Kane

Hivi karibuni kumekuwa na minong'ono ya tetesi zinazomhusisha staa huyo wa kimataifa wa England kuhitajika na Barcelona kwa ajili ya kuziba pengo la Robert Lewandowski anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu.

Kane amekuwa katika kiwango bora tangu atue Bayern ambayo ina mkataba naye hadi mwaka 2027.

Katika msimu huu, Kane amefunga mabao 24 katika mechi 20 zote za mashindano na kuiwezesha Bayern kuwa kileleni mwa msimamo wa Bundesliga kwa tofauti ya pointi nane.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 aliiwezesha timu hiyo inayonolewa na kocha Vincent Kompany kushinda mabao 3-1 dhidi ya St. Pauli Jumamosi baada ya kupoteza dhidi ya Arsenal Jumatano ya wiki iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kane pia amekuwa na mchango mkubwa kwa timu ya taifa ya England ambayo aliiongoza kufuzu Kombe la Dunia 2026, akifunga mabao manane katika mechi nane za kufuzu.

Ripoti zinaeleza Kane, anaweza kuondoka kwa Pauni 56.7 milioni kutokana na kipengele kilichopo katika mkataba wake ambacho kinamruhusu kuondoka mwisho wa msimu huu, lakini kwa sharti la kuipa taarifa Bayern ifikapo Januari kuwa anataka kuondoka katika majira ya kiangazi.

Akizungumza na Sky Sports Germany baada ya Bayern kushinda dhidi ya St. Pauli, Eberl amesema: "Harry anajua kabisa anachotaka na sisi pia bado tuna mipango naye. Tunataka kuendelea naye. Tutafanya mazungumzo zaidi na wawakilishi wake."

Maneno hayo ya Eberl yamekuja baada ya Xavier Vilajoana, anayegombea kiti cha urais cha Barcelona dhidi ya Joan Laporta katika uchaguzi utakaofanyika mwakani kusema kwamba anaweza kumsajili Kane ikiwa atachaguliwa kuiongoza Barca.

"Tuna wachezaji wenye vipaji sana kutoka La Masia, lakini kama tutaona kuna kitu tunakosa, tutajaribu kusajili wachezaji kutoka timu nyingine, kuhusu Kane ikiwa tutaona hakuna mchezaji mwenye sifa kama zake katika timu, bila shida tutamsajili."