Jumanne , 18th Oct , 2016

Beki wa Yanga raia wa Togo, Vincent Bossou amerejea ndani ya kikosi chake kufanya mazoezi kufuatia kuwa nje kwa wiki moja kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

Vincent Bossou

Meneja wa Yanga Hafidh Saleh amesema, Bossou alirejea wiki iliyopita kutoka kuichezea timu yake ya taifa na alishindwa kuingia moja kwa moja kwenye program za timu kutokana na kuanza kuugua malaria.

“Alifika hapa siku tano zilizopita akiwa anasumbuliwa na Malaria, ila kwa sasa anaendelea na amekwishaanza mazoezi,” amesema Hafidh.

Bossou hakuwepo katika mechi mbili zilizopita za Yanga, ikishinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatano na juzi ikilazimishwa sare ya 0-0 na Azam FC, zote katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.