Bwire ataja dawa ya Yanga, "wao wanaruka ruka tu"

Ijumaa , 7th Feb , 2020

Kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kati ya Yanga na Ruvu Shooting, Afisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire amesema kuwa wanayo dawa ya kuwazuia Yanga siku hiyo.

Afisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Masau Bwire amesema kuwa Yanga wajiandae kisaikolojia na mpapaso ambao wataufanya uwanjani siku hiyo.

"Ukiangalia hata uwezo wa wachezaji wao na uwezo tulio nao sisi, hakuna ambacho kinaweza kututisha pale Yanga", amesema.

"Kuna watu nasikia sikia tu wanarukaruka juu ya mpira lakini sisi tunafanya kazi kweli kweli. Tunakwenda kudhihirisha Jumamosi kuwa Ruvu Shooting ni moja ya timu hatari hapa Tanzania, yaani ni Barcelona ya Bongo", ameongeza.

Kwa upande wa Yanga, Afisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli amesema kuwa klabu yao imejiandaa vizuri kuibuka na ushindi na licha ya uwezo wa Ruvu Shooting, wasitarajie watapata matokeo waliyoyapata katika mchezo wa kwanza wa ligi msimu huu.

Mchezo wa kwanza wa ligi uliozikutanisha timu hizo msimu huu, Ruvu Shooting iliibuka na ushindi wa bao 1-0. Katika msimamo wa ligi hivi sasa, Yanga inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34 huku Ruvu Shooting ikiwa katika nafasi ya 9 ikiwa na pointi 26.