
Nadir Haroub (mwenye fulana nyeusi katikati) wakati akiingia kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Nadir Haroub maarufu 'Cannavaro' ambaye ameichezea Yanga kwa miaka 13, akivaa jezi namba 23, amesema kuwa pamoja na uongozi kutaka kuistafisha jezi yake yeye ameona ni vyema iendelee kuwepo lakini mtu anayeivaa aitendee haki zaidi ya alivyofanya yeye.
''Hii jezi namkabidhi Abdallah Shaibu 'Ninja' lakini nachomuomba afanye vizuri zaidi ya nilivyofanya mimi, nimefanya hivi kwa kuwa sitaki jezi hii ipotee uwanjani kwahiyo nina imani na Shaibu kuwa ataendeleza yale mazuri niliyofanya'', amesema.
Nadir Haroub (mwenye fulana nyeusi) akiwaaga wachezaji wa Yanga.
Katika mchezo wa leo Yanga imeshinda bao 1-0 dhidi ya Mawenzi FC, bao likifungwa na mshambuliaji mpya kutoka DR Congo, Heritier Makambo dakika ya 53. Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania amepewa majukumu ya kuwa meneja wa timu hiyo akichukua nafasi ya Hafidh Saleh ambaye amekwenda kuwa mratibu wa timu hiyo.
Canavaro ameshinda mataji 15 na Yanga kuanzia mwaka 2006 alipojiunga nayo akitokea Malindi ya Zanzibar. Ndio mchezaji anayetajwa kuwa amechukua makombe mengi zaidi ndani ya timu hiyo. Ligi kuu mara 8. Ngao ya jamii mara 4, Kagame Cup mara 2 na Azam Federation Cup mara 1.