Ijumaa , 14th Jan , 2022

Kiungo Mshambuliaji raia wa Zambia, Clatous Chama ametangazwa rasmi kama mchezaji mpya wa Simba baada ya kuondoka kwenye dirisha kubwa la Usajili mwaka jana alipojiunga na RS Berkane.

MVP huyo wa Ligi Kuu Tanzania bara, msimu wa mwaka 2019/2020 ametambulishwa mchana wa leo kuwa mchezaji rasmi wa Simba baada ya kufikia makubaliano ya kimkataba na timu yake.

Chama amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na sasa atavaa jezi na 17 iliyokuwa inavaliwa na Pape Ousmane Sakho ambaye sasa atavaa jezi namba 10 iliyokuwa inavaliwa na Ibrahim Ajibu aliyetimukia Azam FC.

Akifaamika kwa jina la ''Mwamba wa Lusaka'' alitimukia nchini Morocco msimu wa 2021/22 akitokea Simba lakini kwenye mkataba wake mpya kulikuwa na suala la kurejea ndani ya timu hiyo ikiwa kutakuwa na makubaliano ya pande zote mbili.

Unakuwa ni usajili wa kwanza kutangazwa rasmi na Simba katika dirisha dogo baada ya tetesi kuwa nyingi kuhusu Chama.

Kwa mujibu wa Seleman Matola, Kocha Msaidizi wa Simba amesema kuwa nyota huyo atawasaidia katika mechi za ligi.

“Chama ni mwenzetu na tutakuwa naye ambapo atatusaidia katika mechi za ligi pamoja na mashindano mengine,”.

Kwenye eneo la kiungo ataungana Rally Bwalya ambaye walitengeneza muunganiko mzuri kutoka na kuelewana vizuri uwanjani na pia itaongeza morali ndani na nje ya uwanja kutokana na uimara na ubora wake.