Jumatano , 6th Aug , 2014

Mashindano ya ngazi za mkoa mwaka huu kuendeshwa kwa mtindo wa mechi za nyumbani na ugenini ambapo mechi za kwanza zitakuwa Septemba 6 na marudiano Septema 13.

Mwakilishi wa Kampuni ya Coca Cola Warda Kimaro(kushoto) akikabidhi vifaa vitakavyotumika kwenye mashindano ya Copa Coca Cola mwaka huu.

Mashindano ya soka kwa vijana walio chini ya miaka 15, Copa Coca Cola, yamepangwa kuanza Septemba 6 mwaka huu na yatachezwa kwa mtindo wa mechi za nyumbani na ugenini.

Kwa mujibu wa droo iliyofanywa na makatibu wa vyama vya soka vya mikoa yote 32 ya Tanzania Bara na Visiwani iliyofanyika uwanja wa Taifa jijini DSM, mkoa wa Kagera utakuwa mwenyeji wa Geita wakati Mara wataikaribisha Mwanza huko Musoma. Siku hiyo hiyo ya Septemba 6 pia Tabora watasafiri kwenda Kigoma na Simiyu watacheza na Shinyanga.

Mchezo mwingine wa fungua dimba utazikutanisha Arusha na Manyara (Manyara) wakati Kilimanjaro watacheza na Tanga.
Michezo mingine itakayochezwa siku hiyo ni Morogoro dhidi ya Pwani, Mtwara dhidi ya Lindi, Njombe dhidi ya Ruvuma, Mbeya dhidi ya Iringa, Rukwa dhidi ya Katavi, Singida dhidi ya Dodoma, kaskazini Pemba dhidi ya Kusini Pemba, Kaskazini Unguja dhidi dhidi ya Kusini Unguja, Ilala dhidi ya Kinondoni na Mjini Magharibi dhidi ya Temeke.

Kitu cha tofauti mwaka huu ni kwamba zaidi ya jezi na mipira kama miaka yote, timu shiriki zimepewa mpaka viatu.