Jumatatu , 1st Feb , 2021

Liverpool wamejipanga kukamilisha usajili wa beki wa kati Ben Davies kutoka Preston North End, kabla ya dirisha dogo kufungwa leo usiku, mabingwa hao wa England wanakabiliwa na majeruhi kwa mabeki wao wa kati. Usajili wa beki huyu utaigharimu Liverpool zaidi ya bilioni 6 za kitanzania.

Ben Davies anatarajia kujiunga na Liverpool kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa leo usiku

Ben Davies mwenye umri wa miaka 25 raia wa England, anatarajiwa kujiunga na klabu ya Liverpool kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 2 akitokea Preston North End, ambayo ni zaidi ya bilioni 6 kwa pesa za kitanzania, lakini pia usajili huo utamuhusisha mchezaji kinda wa Liverpool Sepp van den Berg, ambaye ni beki wa kati, atajiunga na Preston kwa mkopo ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya Liverpool na Preston.

Liverpool wanakabiliwa na majeruhu kwa mabeki wao wa kati wa kikosi cha kwanza Virgil van Dijk, Joe Gomez na Joel Matip. Ambapo kuna muda kocha Jurgen Klopp ilimbidi kuwatumia wachezaji wa safu ya kiungo Jordan Henderson na Fabinho kucheza kwenye eneo hilo la ulinzi.

Klopp pia aliwatumia wachezaji vijana Rhys Williams Nathaniel Phillips ambao kimahitaji wameonekana kutokidhi kulingana na mahitaji ya timu na mashindano wanayoshiriki.

Lakini bado kumekuwa na maswali mengi kama Ben Davies, ataweza kuhimili mikikimikiki ya EPL kwa sababu anatoka kwenye ligi ya daraja la chini Championship.