Ijumaa , 29th Mei , 2020

Hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ASFC imepangwa leo Jijini Dar es Salaam na kushuhudia watani wa jadi nchini, Simba na Yanga wakikutanishwa na wababe wawili tofauti.

Yanga dhidi ya Kagera Sugar

Katika droo hiyo, imeshuhudiwa Simba ikipangwa na Azam FC, mchezo ambao Simba itakuwa mwenyeji huku Yanga wakipangwa na wababe wengine kutoka Kanda ya Ziwa Kagera Sugar. Mechi zingine ni Namungo FC dhidi ya Alliance FC na Sahare All Stars dhidi ya Ndanda FC.

Katika mechi tatu walizokutana Simba na Azam FC msimu huu, Simba imefanikiwa kushinda mechi zote tatu ambapo katika mechi ya Ngao ya Jamii Simba ilishinda kwa mabao 4-2 kisha ikashinda 1-0 na 3-2 kwenye ligi lakini haifanyi mechi hii kuwa rahisi kutokana na ubora wa kikosi cha Azam FC hivi sasa kwani inashika nafasi ya pili katika ligi.

Kwa upande wa Yanga na Kagera Sugar zimekutana mara moja katika ligi msimu huu, kwenye Uwanja wa Uhuru ambapo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na kupelekea mgogoro mkubwa kati ya mashabiki wa Yanga na klabu yao.