Tukio hilo linatarajiwa kufanyika katika ukumbi maarufu wa John F. Kennedy Center for the Performing Arts mjini Washington, D.C., ambapo wadau wakuu wa soka duniani, viongozi wa FIFA na wageni mashuhuri watashiriki. Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria ni Rais wa Marekani, Donald Trump, jambo linaloongeza uzito wa hafla hiyo ya kimataifa.
Hafla hiyo itaaanza saa 12:00 jioni kwa saa za Marekani (ET), ambayo ni sawa na saa 8:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki (EAT). Wakati huo mabalozi wa FIFA pamoja na wawakilishi wa miji16 itakayokuwa wenyeji wa michuano hiyo watashiriki katika mchakato wa kupanga makundi.
Kwa kuwa idadi ya timu imeongezeka hadi 48, mfumo mpya wa makundi 12 yenye timu nne kila moja utatumika, na upangaji utafanywa kwa kutumia "pots" nne kulingana na viwango na vigezo vya FIFA.
Mashabiki wa kandanda kote Afrika Mashariki wanatarajiwa kufuatilia kwa hamu kuona ni timu zipi zitakazokutana katika hatua ya makundi, hatua ambayo inaashiria mwanzo wa safari ndefu kuelekea mashindano makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika historia ya Kombe la Dunia.

