Ijumaa , 10th Sep , 2021

Muingereza Emma Raducanu mwenye miaka 18 amefanikiwa kutinga fainali ya michuano mikubwa Grand Slam ya US Open kwa kumfunga Maria Sakkari kwa seti 2-0 baada ya ushindi wa mizunguko miwili kwa 6-1 na 6-4 na kuwa muingereza wa kwanza kutinga fainali ya Grand Slam tokea Virginia Wade 1977.

Emma Raducanu (kushoto) na Leyla Fernandes (kulia) wakiwa kwenye michezo yao ya nusu fainali kabla ya kutinga fainali usiku wa kuamkia leo Septemba 10, 2021.

Emma ambaye alikuwa anashiriki michuano hiyo kwa mara yake ya kwanza, amezidi kuwa gumzo kufuatia kuonesha kiwango safi tokea aanze kwenye hatua ya kuwanfia kufuzu michuano hiyo na tokea mashindano hayo yaanze amekuwa mchezaji pekee kupata ushindi wa seti 2-0 kwenye michezo yake yote mitano aliyocheza hadi kutinga fainali.

Kwa upande mwingine, Leyla Fernandes wa Canada na yeye amefanikiwa kutinga hatua ya fainali hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kumchapa Aryna Sabalenka ambaye anashika nafasi ya pili kwenye viwango vya ubora Duniani kwa wanawake kwa seti 2-1 ushindi wa 7-6 (7-3), 4-6 na 6-4.

Leyla anatajwa kuwa kwenye kiwango bora cha maisha yake tena hata kupigiwa upatu wa kuibuka na ushindi kwenye fainali baada ya kuwang'oa vigogo watatu kwenye hatua za awali za mtoano hadi kufika fainali hiyo akiwemo bingwa mtetezi wa US Open Naomi Osaka nafasi ya tatu kwa ubora, Elina Svitolina anayeshikilia nafasi ya tano na Aryna Sabalenka anayeshika nafasi ya pili kwa ubora Duniani.

Wawili hao wanatazamiwa kutoa fainali yenye upinzani mkali na wakuvutia baada ya kuonesha viwango bora kabisa hata kwa wachezaji wenye ukomavu zaidi yao kwenye mchezo unaotaraji kuchezwa Septemba 12, 2021 nchini Marekani.

Baada ya kutinga fainali hiyo, Emma Badru ameweka rekodi tele kama vile, Mcheza tenisi wa Engkand mwenye umri mdogo zaidi kufika fainali ya US Open baada ya Christine Truman aliyetinga fainali ya French Open akiwa na miaka 18 mwaka 1959 na kuwa Mwanamke muingereza wa kwanza kufika fainali ya Grand Slam kwenye zama za siku hizi.

Emma anataraji kupanda kwenye viwango vya ubora hadi kuingia kwenye 30 bora kutoka kwenye nafasi ya 150 aliyokuwa nayo na hata Leyla Fernandes kutoka kwenye 336 kwenye michezo ya kuwania kufuzu hadi ndani ya 50 bora.