Jumatatu , 13th Aug , 2018

Nyota wa zamani wa Cameroon Samuel Eto'o mwenye miaka 37, amethibitisha kuwa yupo kwenye mazungumzo na klabu kadhaa za Ufaransa akiwa na mpango wa kucheza ligi hiyo kwa miaka miwili ijayo kabla ya kustaafu rasmi.

Samuel Eto'o

Eto'o ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Cameroon akifunga mabao 56 kwenye mechi 118 alizocheza kwenye timu ya taifa, endapo atapata timu basi itakuwa ni ya 13 katika maisha yake ya soka ambapo safari yake ilianza zaidi miaka 20 iliyopita katika klabu ya Real Madrid mwaka 1997.

Hata hivyo Eto'o hakufanikiwa sana na Real Madrid kabla ya dunia kumtambua zaidi katika miaka 2004 na 2009 akiichezea Barcelona ambako alifunga mabao 130 katika michezo 199 huku akishinda La Liga mara 2 na UEFA mara 2. Mbali na Barcelona Eto'o alipata mafanikio ya kutwaa Serie A na UEFA akiwa na Inter Milan msimu wa 2009/10 chini ya kocha Jose Mourinho.

Mbali na kucheza ligi za La Liga na Serie A, Eto'o ni moja ya wachezaji wachache ambao wamebahatika kucheza ligi kubwa tatu duniani, akicheza pia kwenye ligi kuu ya England katika klabu za Chelsea na Everton na kumfanya awe amechezea klabu 12 zikiwemo mbili za Uturuki Antalyaspor na Konyaspor.

Mwaka 2011 Eto'o aliweka rekodi ya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani alipotoka Inter Milan na kujiunga na Anzhi Makhachkala ya Urusi. Hata hivyo mara baada ya nyota huyo kuweka wazi mpango wake huo klabu kadhaa ikiwemo PSG zimeripotiwa kuwa huenda ndio yupo nayo kwenye mazungumzo.

Eto'o ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye miaka 37 ambao bado wanataka kucheza soka la ushindani na huenda mpango wake ukatimia kwani dirisha la usajili nchini Ufaransa linafungwa Agosti 31 saa 6:00 usiku. Licha ya kutokuwa na timu kwasasa lakini Eto'o anatajwa kuwa na thamani ya Euro milioni 1 zaidi ya shilingi bilioni 26.