Fahamu wachezaji waliogoma kuripoti mazoezini

Alhamisi , 11th Jul , 2019

Ikiwa ni takribani mwezi mmoja umebaki kabla ya Ligi mbalimbali za soka barani Ulaya kuanza, vilabu vipo kwenye maandalizi ya msimu wa 2019/20 ambao kwa nchini England unaanza rasmi Agost 9, 2019.

Neymar Jr

Wafuatao ni baadhi ya wachezaji ambao wamegoma kuripoti kwenye mazoezi licha ya timu zao kuingia kambini.

Kinara wa wote ni Neymar Jr ambaye anakipiga na klabu ya PSG ambayo iliingia kambini Jumatatu Julai 8, 2019.
Neymar ambaye yupo mapumzikoni kwao Brazil hajaripoti bila taarifa yoyote huku akihusishwa na kuondoka klabuni hapo na kujiunga na timu yake ya zamani Barcelona.

Tayari uongozi wa PSG umeshatoa taarifa kuwa utamchukulia hatua za kinidhamu staa huyo kwa kumkata bonasi ya mshahara wake ambayo inakadiliwa kufikia Pauni 100,000 ( Tsh Milioni 287).

Hata hivyo ripoti kutoka Brazil zinaeleza kuwa, Neymar alitoa taarifa kwa uongozi wa PSG kuwa atarejea klabuni ifikapo Julai 15, kwani Julai 13, atakuwa anahudhuria tamasha lake ambalo huwa ni maalum kwa kuchangia wasiojiweza.

Kinara mwingine wa kuchelewa kuripoti ni nyota wa Atletico Madrid Antoine Griezmann, ambaye yeye ameshaweka wazi tangu mwisho wa msimu uliopita kuwa anaondoka.

Griezmann naye hajaripoti kwenye mazoezi pale Wanda Metropolitano licha ya kuhitajika kufanya hivyo kuanzia Jumapili Julai 7, 2019. Griz anahusishwa kujiunga na vilabu vya Barcelona na Man United.

Mwingine anaweza kuwa anashangaza zaidi kutokana na umri wake. Huyu ni mlinzi wa kati ya Arsenal Laurent Koscielny mwenye umri wa miaka 33. Yeye amegoma kusafiri kwenda Marekani kwaajili ya Pre-Season akiwa na Arsenal.

Raia huyo wa Ufaransa anadai alishaiambia klabu kuwa hana mpango wa kuendelea kucheza hapo msimu huu hivyo anataka kuondoka.

Arsenal wameeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha Laurent Koscielny ambaye mkataba wake unafikia ukomo ifikapo Juni 30, 2020.