Ijumaa , 30th Nov , 2018

Mabingwa wa soka nchini, Simba SC wanatarajia kuondoka nchini Jumapili Disemba 2, 2018 kuelekea Botswana kwaajili ya mchezo wake wa marudiano dhidi ya wenyeji wao Mbabane Swallows huku wakiwa na tahadhari za kuepuka vurugu.

Wachezaji wa Simba kushoto na Msemaji Haji Manara

Akiongea leo kuelekea mchezo huo muhimu, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema mchezo huo ni muhimu hivyo kwa namna yoyote watazikabili aina ya fitina zozote zotakazofanywa na wapinzani wao wakiwa na kumbukumbu ya Azam FC kufanyiwa fujo mwaka 2017.

''Msafara wa timu utakuwa na jumla ya wachezaji 21 na viongozi 9 ikiwemo bechi la ufundi na viongozi watahakikisha hakuna kinachoharibika hata kama wapinzani wetu watataka kutuhujuma kama ilivyozoeleka kwenye soka letu'', amesema Manara.

Simba bado wanakumbukumbu ya vurugu ilizofanyiwa Azam FC ilipokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ambapo wachezaji na viongozi wao walikumbana na mashambulizi kutoka kwa mashabiki huku pia wakieleza kutoridhishwa na mazingira ya hoteli waliyofikia.

Kwa upande wa benchi la ufundi Manara amesema wachezaji wote wako vizuri isipokuwa mlinzi wa kulia Shomari Kapombe ambaye anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini.

Kuelekea mchezo huo, Simba wana mtaji wa mabao 4-1 baada ya kupata ushindi huo kwenye uwanja wa taifa katika mchezo wa kwanza. Mabao hayo yalifungwa na John Bocco (mawili), Meddie Kagere na Clatous Chama.