Jumapili , 29th Jul , 2018

Timu ya mpira wa Kikapu ya Flying Dribblers imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kucheza fainali baada ya kufanikiwa kushinda mchezo wake wa kwanza kwenye nusu fainali dhidi ya Team Kiza uliopigwa jioni ya leo Julai 29, kwenye uwanja wa ndani wa taifa.

Flying Dribblers wenye jezi nyeupe kwenye mechi yao dhidi ya Team Kiza

Flying Dribblers ambao mwaka 2017 waliishia hatua ya nusu fainali, wameshinda pointi 84 kwa 75 za Team Kiza, hivyo kuchukua 'game one' kwenye 'Best of three' na endapo watashinda mechi ya pili watafuzu fainali moja kwa moja bila kucheza mechi ya tatu.

Katika mchezo huo mchezaji Habirmana Mayeye wa Flying Dribblers ndio ameibuka kinara kwa kufunga pointi 26, Assist 1 na rebound 4. Kwa upande wa Team Kiza mchezaji Bruno Makombe ameongoza kwa kufunga pointi 17, rebound 15 na Assist 1.

Ili Team Kiza wasonge mbele sasa wanahitaji kushinda mchezo wa pili ili kusawazisha na kwenda kwenye mechi ya tatu ambayo ndio itaamua timu gani iende fainali. Tofauti na hapo watakuwa wameaga mashindano.

Sprite Bball Kings inaandaliwa na East Africa Television LTD, kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite. Bingwa atakabidhiwa shilingi milioni 10 na mshindi wa pili milioni 3 huku mchezaji bora MVP akipoata milioni 2.